Na Ezekiel Kamwaga
AKIANDIKA mapitio ya kitabu cha The Age of Revolutions cha Fareed Zakaria kwenye jarida mashuhuri la Foreign Policy Machi mwaka jana, mchambuzi Michael Hirsh, aliandika mstari mmoja ambao umebaki kwenye kumbukumbu zangu; “Kuna kitu kimeikumba dunia hivi sasa na sote bado hatujajua ni kitu gani”.
Hayo yalikuwa ni mawazo yangu pia wiki hii baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yaliyompa ushindi Tundu Lissu dhidi ya aliyekuwa akishika wadhifa huo, Freeman Mbowe.
Mimi niliamini kwamba hakuna uwezekano wa Lissu kumshinda Mbowe. Siku tatu kabla ya uchaguzi, mmoja wa watu wa karibu na Mbowe alinieleza kwamba ingawa wanahitaji kura 500 tu kushinda uchaguzi, walikuwa na uhakika wa kura walau 700.
Lakini nikaangalia pia katika safu ya juu ya uongozi wa CHADEMA ambako kwa ufuasi, Mbowe alionekana kuwa na watu wengi. Katika uchaguzi wa kanda za chama hicho, wengi wa walioshinda walikuwa watu walionasibishwa na Freeman Mbowe.
Mwenyekiti wa Kampeni wa Mbowe katika uchaguzi huu, Boniface Jacob, alishinda uchaguzi wa kanda yake – ya Mashariki, wakati akiwa ameshikiliwa na mamlaka gerezani. Kama Boniyai anaweza kushinda uchaguzi akiwa jela, anaweza kushindwa kwenye uchaguzi wa ndani ya chama chake akiwa anasimamia mwenyewe? Ndivyo lojiki yangu ilivyokuwa ikiniambia.
Kama Hirsh niliyemzungumzia katika aya ya kwanza, inaonekana mimi na watu wa aina yangu tulikuwa tumepitwa na jambo moja kubwa linaloendelea duniani hivi sasa, kwamba tupo katika zama ambazo upepo unavuma kuelekea kule ambako hatujazoea.
Hesabu zetu kuhusu namba, umahiri wa Mbowe, udhaifu wa Lissu na utaasisi wa mwenyekiti wa zamani aliyedumu madarakani kwa zaidi ya miaka 20, ulitupofusha kuhusu upepo wa mabadiliko uliokuwa unavuma upande wa Lissu.
Kuliko kitu kingine chochote ambacho nitaandika katika uchambuzi huu, sababu kubwa ya ushindi wa Lissu ni kuwa hizi ni zama ambazo ni vigumu sana kushindana na wanasiasa wa aina ya Lissu ambao mimi naamini ni populist kwa kukosa neno mwafaka la Kiswahili kulielezea.
Ni kweli upepo ule ulikuwa unaonekana kuvuma nje ya CHADEMA lakini kwa namna moja au nyingine, wajumbe wa mkutano wa uchaguzi walikuwa wanapata mvumo wake. Haikuwa kazi rahisi kwao kujifanya hawaoni wala kusikia kile kinachoendelea.
Kuna silaha kubwa nne ambazo Lissu – kama ambavyo wanasiasa populists wengine duniani hufanya, Lissu alizitumia ipasavyo kuhakikisha anabadilisha matokeo na kuyageuzia upande wake.
Silaha hizo ni zipi? Silaha hizo ni matumizi ya mitandao ya kijamii, udhaifu wa wanaoshikilia madaraka, jamii iliyogawanyika na kuwapa jina baya washindani wako.
- Udhaifu wa aliyeshika madaraka
Duniani kote inafahamika kwamba wanasiasa pekee wanaoweza kushindana na wanasiasa populists ni wale tu ambao kwenye utawala au uongozi wana cha kujivunia au wanafahamika kwa matokeo.
Kwa mfano, Georgia Meloni na wenzake wa Italia walipata taabu sana kupata mafanikio wakati Matteo Draghi akiwa Waziri Mkuu wa taifa hilo. Ni taabu ambayo Augustine Mrema aliipata wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa.
Kwa kila aina ya uzushi, kashfa au uzembe uliotolewa, Mkapa na akina Draghi huujibu kwa vitendo kuonyesha kwamba kimsingi wao wamefanya vema kuliko hata hao wanaotaka kuchukua nafasi zao.
Tatizo la Freeman Mbowe kwenye uchaguzi huu lilikuwa kwamba ulikuja katika wakati ambao hakuwa na cha kuonyesha kulinganisha na alichokuja nacho Lissu.
Kama siasa za maridhiano alizozipigania zingeweza kuleta mafanikio kwa CHADEMA, labda kwa kukipa chama nafasi katika Baraza la Mawaziri au kupata wabunge kadhaa wa Viti Maalumu bungeni, pengine Mbowe angeonekana tofauti mara hii.
Kama katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka jana CHADEMA ingeibuka na viti vya kutosha walau kukaribiana na vile vya mwaka 2014, huenda Mbowe angeonekana wa tofauti.
Jambo baya kwake lilikuwa kwamba uchaguzi wa mitaa uliofanyika Novemba mwaka jana badala ya kuwa taji katika utawala wake, uligeuka kuwa msumari wa mwisho kwenye jeneza lake la kisiasa. Uchaguzi ule ulikuwa silaha kubwa na zawadi kwa washindani wake ambao ajenda yao ilikuwa kwamba maridhiano ya kisiasa hayakuwa na faida kwa chama hicho.
Suala la maridhiano ya kisiasa lilikuwa ni upanga wenye pande mbili kwa Mbowe, kufanikiwa kwake kungemfanya awe mwanasiasa wa daraja la tofauti nchini lakini kutofanikiwa kwake, kumesababisha awe mgombea mwepesi kwa washindani wake.
- Mitandao ya Kijamii
Mojawapo ya silaha kubwa zaidi kwa wanasiasa populist ni matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii. Wengi wao si vipenzi vya vyombo vya habari vikongwe na kwa sababu hiyo wengi wao hugeukia mitandao.
Jambo lingine kubwa ni kwamba wengi wao huwa hawana ukwasi mkubwa na hivyo huwa hawawezi kumudu gharama za matangazo kwenye vyombo vikongwe vya habari.
Mitandao ya kijamii inawapa mahali pa kupazia sauti zao kwa eneo kubwa na kwa gharama nafuu. Kwenye uchaguzi huu wa CHADEMA, Lissu alitumia ipasavyo mitandao ya kijamii.
Sehemu kubwa ya mahojiano yake aliyafanya mitandaoni na kwenye vyombo vya habari vya mitandaoni. Ni utaratibu huo ndiyo uliougeuza uchaguzi wa CHADEMA kuwa habari ya nchi nzima kwa sababu karibu timu yake nzima ilitumia vema mitandao.
Bila ya mitandao ya kijamii, Lissu na wenzake wasingepata nafasi kubwa ya kujieleza na kueleza wanachotaka kufanya. Bila mitandao, uchaguzi wa CHADEMA usingekuwa mkubwa kama ulivyokuja kuwa.
- Mpasuko katika taasisi
Ni wazi kwamba CHADEMA iliingia katika uchaguzi huu ikiwa haiku pamoja. Aina ya kampeni zilizoendeshwa zilidhihirisha hilo. Timu ya kampeni ya Lissu iliutumia mgawanyiko huo kwa umahiri kuliko ya Mbowe.
Kwa mfano, inaonekana kulikuwa na manung’uniko kuhusu mgawanyo au utolewaji wa nafasi za ubunge wa viti maalumu. Wapo walioamini kwamba kulikuwa na upendeleo.
Kambi ya Lissu ilitumia fursa hiyo kuja na mikakati ya kuhakikisha watu wengi zaidi wananufaika na viti maalumu. Kwa sababu Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA) ilikuwa ikionekana kama ngome muhimu ya Mbowe, hatua ya kusema viti vitagawanywa vizuri zaidi ilimaanisha wanawake wengi zaidi wangeweza kunufaika na Lissu kuliko Mbowe.
Lakini hata wanaume wapiga kura kwenye uchaguzi huo, pengine wana rafiki, ndugu, jamaa na wapenzi ambao wanahisi huenda wenzao hao wangepata nafasi zaidi chini ya Lissu kuliko kwa Mbowe ambako ni kama wabunge wa viti maalumu walikuwa wanajulikana.
Hii ni aina ya mgawanyiko ambao kwa jicho la nje huwezi kuliona lakini lina ushawishi mkubwa kwenye michakato ya kura. BAWACHA inaweza kuwa kwa jumla inamuunga mkono Mbowe lakini kwa fursa za mmoja mmoja, inawezana Lissu aliwagusa zaidi kwa mawazo yake mapya na huenda hilo liliamua matokeo.
- Nguvu ya jina baya
Lissu, kama walivyo wanasiasa wengi wa aina yake, ni mahiri katika siasa za kumpa mtu jina baya au ajenda ambayo ni rahisi kueleweka na likinasa, inakuwa vigumu sana kwa aliyepewa kujinasua.
Kwenye kampeni hizi, ajenda kubwa ya Lissu ilihusu kukithiri kwa rushwa ndani ya chama hicho. Yeye mwenyewe na baadhi ya wafuasi wake, hawakuona haya kuficha majina ya baadhi ya viongozi wa chama hicho waliowatuhumu kujiweka kwenye mazingira ya rushwa.
Bahati mbaya ni kwamba Mbowe hakuwahi kuwa na majibu sahihi ya hoja hii. Bahati mbaya zaidi ni kwamba kila yeye au watu waliokuwa kwenye kambi yake walipojitokeza kutoa ufafanuzi, waliharibu zaidi kuliko kujenga.
Nilishangaa sana pia kwamba watu waliohusishwa naye kwa karibu, kwa mfano Boniyai na Joseph Mbilinyi (Sugu), hawakuwahi kujitokeza hadharani kumtetea Mbowe.
Wakati Godbless Lema na John Heche, miongoni mwa viongozi waandamizi na wanaoaminika wa CHADEMA, walipojitosa kumuunga mkono Lissu, nilitaraji Boniyai na Sugu nao wangetoka hadharani. Hawakutoka na wakawaachia Yericko Nyerere na Paul Ntobi kazi ya kumtetea Mwenyekiti.
Matokeo yakawa kwamba hoja za kambi ya Lissu hazikuwahi kujibiwa kwa uzito uleule wa hoja na mzungumzaji. Mpaka siku ya kupiga kura, picha jongefu yoyote iliyokuwa ikionekana ya mwana CHADEMA kugawa fedha, ilihusishwa na kambi ya Mbowe.
Sina uhakika kama kambi ya Lissu ‘haikuwaona wajumbe’ hasa katika siku ya mwisho ya upigaji kura au wakati wowote kwenye kampeni hii. Hata hivyo, kambi ya Mbowe ilibandikwa chapa ya rushwa na ilibaki hadi siku ya mwisho.
Sababu zote nilizotaja hapo juu, zingekosa nguvu ya kumwondoa Mbowe madarakani kama upepo usingekuwa mkali upande wa Lissu.
Kama kuna kitu ambacho wengi wetu hatukukisoma mapema kwenye kampeni hizi za CHADEMA mwaka huu, basi kitu hicho ni nguvu ya upepo wa kisiasa.
Mwandishi ni Msomi wa Masuala ya Siasa za Maridhiano na ni Mhitimu wa Shahada ya Uzamili katika Siasa za Afrika (African Politics), aliyoipata katika Chuo Kikuu cha London School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza. Anapatikana kupitia email; ekamwaga57@gmail.com

